Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais Maduro sambamba na kukosoa hatua hiyo ya Marekani ya kuwatumia wapinzani wa Venezuela kiasi cha dola milioni 150 ambazo ni sehemu ya fedha za nchi hiyo zilizozuiwa na Washington amesema kuwa, wapinzani wa nchi hiyo wanaoongozwa na Juan Guaido wameacha medani ya siasa na kugeuka kuwa genge la uhalifu.
Maduro amesema kuwa, Guaido na watu wake wa karibu watatumia fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza mwenendo wa kuzusha vurugu na machafuko nchini Venezuela, wakati fedha hizo zilizozuiwa na Marekani ni mali ya wananchi wa Venezuela na zinapaswa kutumika katika kununua dawa, chakula na zana za sekta ya viwanda.
Kinyume na baadhi ya tabiri kuhusiana na kutokea mageuzi katika siasa za Marekani kuhusiana na Venezuela na Rais Maduro katika kipindi cha utawala wa Rais Joe Biden, inaonekana kuwa, Washington imeazimia kuendeleza sera na siasa zile zile zilizoshindwa na kugonga mwamba za Rais aliyetangulia Donald Trump, yaani siasa za kutoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa wapinzani wa Venezuela wanaoongozwa na Juan Guaido. Marekani inaendeleza siasa hizo ikiwa na matumaini ya kuisambaratisha serikali ya mrengo wa kushoto nchini humo inayoongozwa na Maduro.
342/